Rais Trump : 'Tumeanzisha Vita Vikali Dhidi ya Adui Asiyeonekana'

Ifuatayo ni tahiriri inayoelezea sera na msimamo wa serekali ya Marekani.

Katika hotuba yake kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, rais Donald Trump alieleza kuwa ulimwengu upo katika mapambano makubwa duniani: Tumeanzisha vita vikali dhidi ya adui asiyeonekana, virusi vya china ambavyo vimesababisha vifo vingi katika nchi 188”, Trump alisema.

Marekani ilianzisha uhamasishaji mkubwa wa kupambana na COVID-19, ikiwemo kuzalisha vifaa vinavyosaidia wagonjwa wa corona kupumua, vifaa ambavyo viligaiwa kwa mataifa mengine ambayo yanavihitaji na kusaidia katika tiba inayostahili. Kufikia sasa, chanjo tatu ziko katika hatua za mwisho za majaribio, rais Trump alisema.

“Tutagawa chanjo, tutavishinda virusi hivyo, tutatokomeza janga hili, tutaingia kwenye enzi mpya ya ustawi mkubwa, ushirikiano na amani.”

Wakati huo huo, lazima viongozi wa China wawajibishwe kwa vitendo vyao, alieleza rais Trump.

“Katika siku za mwanzo za virusi, China ilifunga safari za ndege za ndani, huku ikiruhusu ndege zake kuondoka China na kwenda kuambukiza mataifa mengine ya dunia. Serikali ya China na Shirika la Afya Duniani (WHO) linalodhibitiwa kabisa na China, lilitangaza kwamba hakuna ushahidi kuwa virusi hivyo vinaambukizwa kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine.”

Rais Trump aliisihi Umoja wa Mataifa kuiwajibisha China kwa vitendo vyake vya kuchafua mazingira.

“Kila mwaka, China inamwaga mamillioni ya tani za plastiki na uchafu baharini, inafanya uvuvi mkubwa kwenye maji ya nchi nyingine, kuharibu maeneo mengi ya miamba ya matumbawe, inatoa gesi yenye sumu ya zebaki angani kuliko nchi yoyote mahali popote duniani. Hewa chafu inayozalishwa na China ni karibu mara mbili ya ile ya Marekani, na inaongezeka haraka.”

Kama Umoja wa Mataifa unataka kuwa taasisi yenye kufanya shughuli zake kwa ufanisi, “linatakiwa kujikita kwenye matatizo ya kweli ya ulimwengu. Ni pamoja na ugaidi, manyanyaso dhidi ya wanawake, kazi za kulazimishwa, ulanguzi wa dawa za kulevya, usafirishaji haramu wa watu na usafirishaji kwa sababu ya masuala ya kingono, mateso ya kidini, na usafishaji wa kikabila kwa dini wa wale walio wachache.”