Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo kupitia taarifa amesema kuwa chama cha kikomunisti cha CCP kinacho tawala China kinalenga kueneza ushawishi wake wa ki-Marxist kote ulimwenguni.
Waziri huyo amesema kuwa mojawapo ya mbinu zinazotumiwa na chama hicho ni kupitia idara maalum ya serikali inayofadhili miradi ndani na nje ya nchi kwa kutumia propaganda na ukandamizaji.
Idara hiyo kwa jina la United Front Work Department hukandamiza wasomi, wafanyabiashara, asasi za kiraia, jamii za wa China zinazoishi kwenye mataifa ya nje wakiwemo wale kutoka makabila ya walio wachache wanaojaribu kukosoa serikali kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu kwenye maeneo ua Xinjiang, Tibet na kwengineko ameongeza Pompeo.
CCP kwa kawaida kinawalenga watu wanaoshukiwa kukipinga huku kikitoa taarifa zao binafsi pamoja na za familia zao kwenye mitandao ya kijamii ikiwa kama mbinu ya kuwakandamiza kisiasa.
Ikiwa kama hatua ya kudhibiti uovu huo, Pompeo ameweka masharti makali kwenye utoaji wa visa za kusafiria kupitia idara ya taifa ya uhamiaji dhidi ya watu wa China na hasa maafisa wa chama cha CCP wakiwemo wale wanaoshukiwa kuhusika kwenye shughuli za idara ya United Front Work.
Miongoni mwao ni wale wanaoshukiwa kutisha watu, kuiba na kutoa taarifa za watu binafsi kwenye mitandao, ujasusi wa taarifa za mataifa ya kigeni, kuingilia siasa za ndani, kukandamiza uhuru wa wasomi pamoja na biashara za watu.
Maovu hayo hufanywa ili kuongeza ushawishi wa CCP kwa viongozi wa kieneo pamoja na ndani ya China, wasomi pamoja na asasi za kiraia hapa Marekani pamoja na kwenye mataifa mengine.
Pompeo ameongeza kusema kuwa ataendelea kuongeza masharti makali ili kutoa ujumbe kwa watenda maovu hao kuwa hawakaribishwi Marekani. Marekani inaomba serikali ya China kusitisha mwenendo huo unaokandamiza uhuru wa kujieleza.