Accessibility links

Breaking News

Maadhimisho ya kuzaliwa Yesu Kristo Duniani


Ifuatayo ni tahariri inayoeleza sera na msimamo wa serikali ya Marekani.

Tarehe 25 mwezi Disemba kila mwaka ni moja ya siku takatifu na muhimu mno kwa Wakristo, ambapo huwa wanaadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo takriban miaka 2000 iliyopita.

Yesu anaenziwa na Wakristo kama mwana wa Mungu aliyefufuka, mwokozi na nuru ya ulimwengu. Wazazi wake, Maria na Yusufu, walikuwa maskini, kama watu wengine kwenye jamii, na inaeezwa kwamba Yesu alizaliwa katika hori la ng’ombe, msimu wa baridi kali.

Tangu jadi, watu wanaoishi katika ukanda wa Kaskazini wa dunia, husherehekea msimu wa baridi, ukiwa ni mwanzo wa siku zenye mwangaza kwa kipindi kirefu, na matuamaini ya ufufuo wa mazingira. Watu wa zamani kote duniani walikaribisha mwaka mpya kwa hafla mbalimbali. Kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo karibu na kipindi hicho, kulifanyika katika mazingira ambayo hadi leo, yanashuhudiwa kwenye baadhi ya jamii kote duniani.

Takriban siku tatu kabla ya sikukuu ya Krismasi, Wachina na jamii zingine za mashariki mwa Asia, huadhimisha siku kuu ya Dongzi, ambapo familia hukusanyika pamoja na kukumbuka mwaka uliokwisha, na kadhalika kusherehekea mwanzo wa msimu wa baridi na ujio wa mwangaza.

Sherehe ya jadi iitwayo Yalda nayo ni muhimu mno kwa raia wa Iran, huku Wajapan nao wakiadhimisha sikukuu ya Toji, ambayo, kiutamaduni, husherehekewa kama njia ya kuukaribisha mwaka mpya kwa afya bora na kuwatakia watu bahati nzuri.

Ingawa maadhimisho yote hayo yanatofautiana kwa njia moja au nyingine, hali ya kuchangamka na kuwa na matumaini ni Dhahiri kwa kila jamii. Kwa Wakristo, kinachoendelea kukumbukwa karne zote ni jinsi malaika alivyotangaza katika usiku wa kwanza wa Krismasi, kuhusu kuzaliwa kwa mtoto ambaye angeleta matumaini na amani duniani.

“Kila mwaka, wakati wa krismasi, tunatambua kuwa moyo halisi wa Krismasi siyo mali tuliyo nayo, bali ni kutambua sisi ni nani, kwamba kila mmoja wetu ni mwana wa Mungu. Hicho ndicho chanzo halisi cha furaha msimu huu, na hicho ndicho kiifanya Krismasi iwe ni wakati wa furaha,” alisema rais wa Marekani Donald Trump.

Tunaomba kwamba nchi yetu itakuwa pahala ambapo kila mtoto anaishi katika nyumba iliyojaa mapenzi, jamii iliyojaa matumaini, na nchi iliyojaa imani, aliongeza Rais Trump.

…Hiyo imekuwa ni tahariri iliyoelezea sera na msimamo wa serikali ya Marekani.

XS
SM
MD
LG