Marekani inaendelea kulilenga kundi la kigaidi la al-Qaida pamoja na washirika wake likiwemo kundi la al- Shabaab. Hivi karibuni wizara ya mambo ya nje ya Marekani imewaorodhesha viongozi wawili wa al-Shabaab Abdullahi Osman Mohamed na Maalim Ayman kama magaidi wa kimataifa wanaosakwa.
Abdullahi Osman Mohamed anaejulikana pia kama Mhandisi Ismail, ni mtaalam wa vilipuzi kwenye kundi hilo na anahusika katika kuratibu, kuongoza operesheni pamoja na utengenezaji wa vilipuzi. Mohamed pia ni mshauri maalum wa kiongozi wa kundi hilo na pia mkuu wa kitengo cha habari al-Kataib.
Maalim Ayman ndiye kiongozi wa Jaysh Ayman ambacho ni kitengo cha al-Shabaab kinachoongoza mashambulizi ya kigaidi nchini Kenya na Somalia. Ayman alihusika kupanga shambulizi la Januari mwaka huu kwenye kambi ya kijeshi ya Simba ilioko Manda Bay nchini Kenya, ambapo mwanajeshi mmoja pamoja na wakandarasi wawili kutoka Marekani waliuwawa.
Al-Shabaab liliorodheshwa kama taasisi ya kigaidi Machi 2008 na limeendelea kuwa tishio la amani, usalama na uthabiti wa Somalia pamoja na Kenya.
Kupitia taarifa iliotolewa, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema, “ Marekani ina nia ya dhati kuvuruga mbinu haramu za al- Shabaab za kuchangisha fedha, kuzuia uwezo wake wa kufanya mashambulizi zaidi dhidi ya raia pamoja na kushirikiana na serikali kuu ya Somalia katika kuvuruga ufadhili wa kundi hilo. Hili litahitaji ushirikiano wa karibu ili kuzima uwezo na operesheni za kundi hilo, kupambana na udhibiti na ushawishi wake kwenye eneo la Afrika mashariki.”
Kutokana na hatua zilizochukuliwa na Marekani, raia wa Marekani wamezuiliwa kujihusisha na njia yoyote ile na Mohamed pamoja na Ayman. Mali zao zilizoko kwenye maeneo yanayomilikiwa na Marekani pia zimezuiliwa. Ni uhalifu kwa mtu yeyote akifahamu fika kutoa taarifa au kujaribu kulisaidia kundi la al- Shabaab kwa namna moja au nyingine.
Nathan Sales mratibu wa maswala ya kupambana na ugaidi hapa Marekani anasema kuwa hatua zilizochukuliwa pia zinazuia ugaidi wa kimataifa na kwamba wanafanya kila juhudi kukabiliana na tatizo hilo siyo tu kwa kuwawekea wahusika vikwazo mbali pia kuzuia usafiri pamoja na ushirikiano ili kulinda sehemu zinazoweza kushambuliwa kwa urahisi.
Sales ameongeza kusema kuwa Marekani iko tayari kushambulia kundi lolote la kigaidi lililoko nje ya nchi na ambalo ni tishio kwa raia wake na mali zao zilizoko kwenye mataifa ya kigeni au washirika wake. Anasema kuwa wanalenga kusambaratisha juhudi za makundi kama al-Shabaab kwa hatua kadhaa ambazo wanaamini zitafanya kazi.