Marekani inataka kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaosomea Marekani wanakuwa na uwezo wa kutambua iwapo lugha za kichina na masomo kuhusu utamaduni yanayotolewa shuleni yana nia ya kubadilisha mawazo yao kwa njia ya ujanja kwa misingi ya chama cha kikomunisti na washirika wake.
Hatua ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani kutambua taasisi ya Confucius ya hapa Marekani – CIUS, kama ofisi ya mambo ya kigeni ya serikali ya China, inatambua uhalisi wa taasisi hiyo.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, amesema kwamba taasisi hiyo inaendeleza propaganda ya Beijing kupitia shule za msingi, upili na vyuo vya Marekani.
Taasisi ya Confucius inadhaminiwa na serikali ya China ni sehemu ya juhudi za kueneza propaganda kote duniani za chama kinachotawala nchini China, cha Kikomunisti.
Utambuzi huo hautapelekea taasisi ya CIUS kufungwa au kutoa masharti kwa vyuo au vyuo vikuu kuifunga. Badala yake, hatua hiyo itahakikisha kwamba kuna uwazi kwa kuhakikisha kwamba taasisi hiyo inatoa taarifa za kila mara kwama wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuhusu wafanyakazi wake ambao ni raia wa China, namna wanavyoajiri watu kazi, ufadhili wake na shughuli zake zote ndani ya Marekani.
Kwa kutoa habari hizo, shule za Marekani zitakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya uhakika na kujua iwapo kuna ushawishi dhidi yake na iwapo mipango inayofadhiliwa na Beijing inastahili kuendelea kutoa elimu kwa wanafunzi wake.
Kulingana na muungano wa kitaifa wa wasomi – NAS, kuna taasisi 75 za Confucious nchini Marekani.
Kuna karibu madarasa 500 za Confucius katika shule za msingi na idadi kubwa zina uhusiano na mojawapo ya chuo kikuu chenye ushirikiano na taasisi za Confucius.
Ushawishi wa serikali ya China na athari za ushawishi wa chama cha kikomunisti cha China kuhusu mipango ya taasisi za Confucius vimepelekea kuwepo kwa hali ya wasiwasi kutaka kujua mchango wake kwa vyuo vya Marekani.
Kwa mfano, ripoti ya mwaka 2017 kuhusu taasisi za Confucius au Cis na NAS, zilibaini kwamba baadhi ya vitivo vya CI vinapata shinikizo vya kujizuia; mikataba kati ya Cis na vyuo haijulikani hadharani; baadhi ya vyuo vikuu vinapewa pesa ili kutokosoa PR; na masomo yanaotolewa na CI mara nyingi yanatoa elimu isiyo kamilifu kuhusu historia ya China kwa kutozungumzia swala la ukiukwaji wa haki za kibinadamu.
Naibu wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayeshughulikia mambo ya mashariki mwa Asia na Pacific David Stilwell, amesema kwamba kwa zaidi ya miongo minne, Beijing imefurahia mazingira ya wazi na uhuru wa kuingia katika jamii ya Marekani, huku ikikosa kutoa mazingira kama hayo kwa Marekani na nchi zingine na kwamba Uhusiano huo hauna usawa kabisa, akiongezea kwamba lengo la Marekani ni kutaka China kuelewa umuhimu wa uwazi, na ushirikiano. Na hadi hilo litakapofanikiwa, tutachukua hatua za kujilinda wenyewe.